Wednesday 29 May 2013

TATIZO SIO SURA NI KUJIKATAA MWENYEWE!


                                                  Na Frt. Carlos Mlelwa

Baada ya kukaa na kutafakari kwa makini maswala ambayo yanafanywa na baadhi ya watu, sikuwa na subira ya kuvumilia zaidi. Niliona ni bora nikae na kuandika hoja hii. Sio kwamba nilifuraishwa sana na hali ambayo niliiona bali nilifikiri kwa muda mrefu bila kupata sababu za kimsingi za mambo niliyoyaona yakifanywa na watu. Ni katika hali ya mtizamo wa kisaikolojia na kibaolojia niliamua kuchambua niliyoyaona na kuyasikia kutoka kwa watu mbalimbali.
Sio jambo jipya ninalotaka kulizungumzia hapa, bali ni la kawaida kwa baadhi ya watu na la masikitiko kwa watu wengine. Jambo lenyewe sio lingine bali ni suala zima la Kujichubua. Kujichubua ni hali ya kutumia aina fulani za vipodozi au mkologo katika kubadili rangi ya ngozi asilia ya mwanadamu.
Ni ujinga, na tena ni kukosa maarifa kwa mtu kutaka kufanana na mtu mwingine ambaye kapendezwa naye kisura. Nasema kuwa ni ujinga na tena ni jambo la ajabu sana kwa sababu kuu mbili kama mtu ana akili timamu.
Sababu ya kwanza ni kwamba, katika dunia hii ni wewe tu una sura uliyo nayo na wala hamna mtu mwingine anayefanana na wewe kwa asilimia mia moja. Sasa ni kwanini mtu huyu asijivunie upekee wake alio nao? Ambaye anakataa upekee wa sura yake anataka kusambaza upekee  wa sura ya mtu anayedhani ni bora zaidi.




OOO!! MY AFRICA
Sababu ya pili ni kwamba, kuna uelewa mdogo sana wa watu wanaojibadili sura zao kiasilia. Kwa asili kuna mambo ambayo yapo kama yalivyo na kuyabadili ni kujiletea matatizo katika maisha yako.
Hali kadhalika na sura ya mtu pekee kwa ajili yake tu, kuibadili ni ndoto. Hata kama atajitahidi kwa nguvu zake zote kujibadili, sura ile itabakia palepale na wewe kama wewe haitakaa itokee hata siku moja watu waseme wewe ni Asha wakati wewe ni Mwajuma au ni Hamisi wakati ni Juma.
Kwa wale wanaofahamu thamani ya mtu ni mtu mwenyewe, watakushangaa kwa jinsi usivyotaka upekee wako na kukimbilia upekee wa watu wengine.

Kila mtu kwa jinsi alivyo, yatosha kabisa kumtambua yeye kama yeye na sio kama yule. Mtu anavyojitahidi kujibadili kwa kutumia njia sisizo sahihi na kwa malengo yasiyo sahihi, basi mtu huyu kajikataa yeye kama yeye na bila shaka amewakataa na wazazi wake walio mleta hapa duniani.
Watu wengi hujichubua ili kubadili muonekano wa nje wa ngozi za miili yao. Watu walio wengi hujichubua kwa malengo ya kuonekana wazuri mbele za watu. Mwanzoni, dada zetu ndio walipenda zaidi kujichubua ukilinganisha na wanaume.
Hata hivyo, waliojichubua ni wale waliokuwa katika mazingira ya mijini na vijijini kwa kiasi kidogo. Walifanya hivyo ili kubadili muonekano wa nje wa ngozi zao ufanane na walivyotaka wao kwa kutumia vipodozi mbalimbali kutoka mataifa ya nje.
Kwa sasa, kinachonishangaza hata wanaume nao hujichubua kwa malengo kama ya baadhi ya akina dada. Ni mambo ya ajabu sana! ambayo kwa kizazi cha sasa imekuwa kawaida, ila zamani mambo haya hayakuwepo na watu walipendana na ndoa zilikuwa imara kuliko ilivyo katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.


Sio kila kitu ni cha kutumia eti kwa sababu kimetoka Ulaya au Marekani. Pia sio vizuri kufanya mambo kwa kuiga bila kujua madhara yake. Haipendezi mtu kujichukia mwenyewe. Kila mtu anao uzuri wake wa kipekee tofauti na wa mtu mwingine.
Kila mtu pia kwa jinsi alivyo anaye mtu anayempenda labda tu haujafikia muda wake. Kujichubua ili kupata mchumba ni sawa na kujiharibia sifa ya uzuri wako. Kujichubua ili kufanana na mtu mwingine ni sawa pia na kupiga rangi upepo maana kila mtu ni tofauti na mwenzake, na wala hamna watu wanaofanana kwa kila kitu hata kama ni mapacha wanaofanana (identical twins). Kuna faida gani kwa mtu kujichubua halafu ajiharibie asili yake? Au ni faida gani ya mtu kujichubua halafu adharaulike na jamii?
Watu wanaojichubua wako katika hali mbili. Kuna wale ambao wakijichubua hupendeza kwa muda mfupi na kuna wale ambao wakijichubua huwa ni kituko cha mwaka! Afadhali ya kinyago ni kizuri! Faida ni ndogo sana kwa wale ambao hijichubua ukilinganisha na madhara wanayoyapata.
Faida mojawapo ni kwa aliyejichubua kujiona mzuri na nyingine ni kwa watu kuusifu uzuri bandia utokanao na mtu aliyejichubua. Madhara ya kujichubua ni mengi mno, tena kisaikolojia na kibaolojia. Kwa mfano, mtu aliyejichubua kisaikolojia hajiamini yeye na sura yake.


Hivyo, muda mwingi huwa katika mazingira ya kuangalia maendeleo ya ngozi yake. Kama amejichubua na akakosa alilolitaka kama vile mchumba, huumia sana rohoni, na kama atafanikiwa itabidi atumie gharama zaidi ili kujitunza na hii hupelekea  kufikiri zaidi juu ya mwili kuliko kazi. Kibalojia, mtu aliyejichubua huenda akapatwa na magonjwa mbalimbali ya ngozi kama maupele, kansa ya ngozi, nywele kunyonyoka, makovu na kupungua kwa kinga ya mwili na kuchangia vifo katika umri mdogo.
Ni vyema, tena ni vyema sana, kutambua kuwa, kwa jinsi tulivyo ni wazuri na hatuhitaji uzuri mwingine kwani aliyetuumba ana sababu zake na kwenda nje ya sababu hizo ni sawa na kujitia kitanzi. Kila jambo ni jambo kama lina faida inayodumu kwa mwanadamu ila jambo sio jambo kama lina madhara kwa mwanadamu. Tujivunie Uafrika wetu, tuachane na kujitafutia uzuri feki wa kujiua wenyewe.
Tangu nizaliwe tumboni mwa mama yangu, sijawahi kumwona Mzungu anajishughulisha na vipodozi kwakutaka kuibadilisha ngozi yake ili ifanane na Mwafrika! Hii ni kwasababu anaipenda na kuithamini ngozi yake. Kwanini itokee kwako wewe Mwafrika? Hivi hii ni laana au…!! Hey! Waafrika, yanatuingia kweli akilini!


0 comments: